Na Mwandishi wetu.
JESHI la Zimamoto Mkoa wa Simiyu leo limeungana kuadhimisha Siku ya Wazimamoto Duniani katika maonyesho yaliyofanyika kwenye Kiwanja cha Sabasaba (CCM), wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambapo wananchi, wanafunzi na makundi mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kupata Elimu ya Zimamoto.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Simiyu, Mrakibu Msaidizi Faustin Mtitu, amesisitiza umuhimu wa elimu ya kujikinga na majanga ya moto, akiwahimiza wananchi kushiriki kwa karibu kujifunza mbinu za uokoaji na usalama.
Maadhimisho hayo yameambatana na maonyesho ya vitendo vya kuzima moto, mafunzo ya uokoaji na matumizi ya vifaa vya zimamoto, pamoja na burudani ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu ambapo Raha Queens waliibuka washindi wa mabao 2–0 dhidi ya Kidinda Girls.
Wananchi wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kupongeza elimu hiyo muhimu, wakisisitiza kuwa imewapa uelewa zaidi wa kukabiliana na majanga ya moto.
Siku ya Wazimamoto Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Mei, ikiwa ni siku ya kutambua mchango wa wazimamoto na kuhamasisha usalama dhidi ya moto duniani kote.
Mwisho.














0 Comments