MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga (katikati) akizungumza kwenye Kikao cha kuhamasisha chanjo ya polio.

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bariadi, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Simon Simalenga amelionya Kanisa la Last Church of God kuzuia watoto kupata chanjo ya polio inayotekelezwa na serikali kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 kwa awamu ya pili katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Singida.

Aidha, Simalenga amesema serikali inaendelea kushirikiana na Madhehehu ya dini katika shughuli mbalimbali za kijamii lakini kanisa hilo limekuwa likizuia watoto kupata chanjo kwa madai kuwa siku moja watu wote watakufa na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka Sheria za nchi na kuhatarisha Usalama wa watu.

Akizungumza leo kwenye Kikao cha Uhamasishaji wa kampeni ya chanjo ya Polio awamu ya pili, Simalenga amesema kuwa Makanisa na Taasisi zingine za dini zinafanya vizuri sana kutekeleza majukumu yao huku akilionya kanisa hilo kutoharibu Mipango ya serikali katika kutimiza majukumu yake kuwahudumia wananchi.


"Ipo Taasisi ya dini, Kanisa la Last Church of God, kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikienda kinyume na maelekezo, taratibu na miongozo iliyoanzisha Taasisi hiyo...mwaka juzi walisababisha vifo vya watoto wawili baada ya zoezi la chanjo ya nyumba kwa nyumba, walizuia chanjo kuwa tutakufa tu" amesema.

''Tulichukua hatua na miongoni mwa hatua hizo ni kuyaita Makanisa hayo kuwahoji kuhusu utaratibu wao, tuliwataka kutekeleza maagizo ya serikali ikiwemo chanjo kwa watoto sababu ni Wajibu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha tunawalinda watu wote." Amesema na kuongeza.

"Hatutaki mtu afe kwa sababu tutakufa, huwezi kujiita kiongozi wa dini kama hakuna taratibu zinazokutambulisha kwa mujibu wa sherja za nchi... serikali inataka kuwahudumia watu wake, wewe unasema hapana, tuhakikishe tunao Wajibu wa kuwalinda wananchi wetu" 

Sambamba na hayo, Simalenga amesema kuwa zoezi la chanjo awamu ya kwanza katika wilaya hiyo, lilifanyika vizuri na kwamba hakuna mgonjwa wa ugonjwa wa polio katika eneo hilo huku kampeni hiyo imehusisha viongozi wa dini, waganga wa tiba asili ma tiba mbadala. 

Mchungaji wa kanisa la Last Church of God kutoka kijiji Cha Nyamswa, Mathayo Samweli Nkinda amesema awali kanisa lao lilikuwa la Walokole (Watolamhali) yaani kanisa la ndoa ya wake wengi, lakini baada ya kuingia Askofu mpya alibadili katiba. 

"Kuna Last Church za aina mbili, ya kuoa mke mmoja na nyingine ya kuoa wake wengi, alipoingia Askofu mpya, katiba iligeuka na kuwa ya kuoa mke mmoja, wengine walipinga na kubaki na wake wawili.. Last church ya wake wawili bado wanapinga dawa na chanjo, lakini sisi wa mke mmoja hatupingi dawa wala chanjo" amesema.

Mwalimu Daud Jackson kutoka Shule ya Wasabato Bupandagila, amewataka viongozi wa dini kuruhusu kanuni za matabibu ili watibu wanadamu bila kuzuiwa kupitia imani za dini huku akiwataka wadau kuunga mkono kampeni ya polio kwa Afya ya vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Lameck Mkilila ameipongeza serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Bariadi kwa kuonya Taasisi za dini kuzuia chanjo ya Serikali ambayo inalenga kustawisha jamii.

Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Pilia Zambi amesema kuwa zoezi hilo la chanjo awamu ya pili linatarajia kufanyika Mei 7 mpaka 10 na kwamba wanatarajia kuwafikia watoto 178,793 ambapo awamu ya kwanza walifikia watoto 159,000 sawa na asilimia 112.

Amewataka wazazi, jamii na walezi kuruhusu watoto kupata chanjo ili waweze kujikinga na ugonjwa wa polio ambapo huduma zitatolewa shuleni, makanisani, misikitini, majumbani na sehemu zozote ambazo mtoto atakuwa anapatikana.

Mwisho.