Na Samwel Mwanga.
KAMISHNA wa jeshi la Magereza,Amina Kavirondo ambaye ni Kamishna wa Huduma na Urekebu wa Jeshi hilo amewaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP)mstaafu,Shaku Umba.
Mazishi hayo yamefanyika April 18,2026 katika makaburi ya Mzumbe, Mtaa wa Vikenge 280 mkoani Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini,Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Godfrey Boniface Kavishe, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa wa Morogoro,ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu,jamaa na marafiki, akieleza kuwa Jeshi limepoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika utumishi wa umma.
“Tumempoteza mtumishi aliyekuwa na nidhamu ya hali ya juu na aliyejitolea kwa dhati katika kulijenga Jeshi la Magereza. Mchango wake utaendelea kukumbukwa,” amesema.
Katika mazishi hayo ya kijeshi, viongozi mbalimbali wastaafu wa Jeshi la Magereza walihudhuria, wakiwemo Wakuu wa Jeshi la Magereza Nchini, wastaafu Dk Juma Malewa na Ramadhan Nyamka,.
Pia alikuwepo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza(SACP), mstaafu Mussa Kaswaka pamoja na Kamishna Msaidizi wa Magereza( ACP) mstaafu Haseed Mkwanda.
Katika uhai wake, marehemu Umba aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Magereza, ikiwemo Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Maswa, Butimba mkoani Mwanza,Musoma mkoa wa Mara pamoja na kuwa Mkuu wa Magereza katika mikoa ya Shinyanga na Singida.
Baadhi ya askari waliowahi kufanya kazi na marehemu walieleza kuguswa na kifo hicho, wakimtaja kuwa kiongozi aliyekuwa karibu na watumishi wake na mwenye kusimamia nidhamu na haki kwa vitendo.
“Alikuwa kiongozi wa mfano, aliyethamini watu wake na kusimamia maadili ya kazi bila kuyumba. Pengo lake si rahisi kuzibwa,” alisema mmoja wa askari hao.
Kwa upande wa familia, ndugu wa marehemu walieleza masikitiko yao makubwa kufuatia msiba huo, huku wakishukuru faraja na mshikamano walioupata kutoka kwa viongozi na wananchi waliojitokeza katika kipindi chote cha maombolezo.
“Ni pigo kubwa kwetu, lakini tunafarijika kuona namna alivyogusa maisha ya watu wengi. Tutamkumbuka kwa upendo na malezi aliyotuachia,” alisema mmoja wa ndugu wa familia.
Naye Ally Omary mkazi wa wilaya ya Maswa alikowahi kufanya kazi marehemu, alimwelezea kuwa kiongozi aliyekuwa karibu na jamii na kushirikiana vyema na wananchi katika shughuli za maendeleo.
“Alikuwa mtu wa watu, hakujitenga. Alishirikiana nasi katika mambo ya kijamii na maendeleo. Leo tunamkumbuka kwa unyenyekevu wake,” amesema.
Mazishi hayo yameacha pengo kubwa si tu kwa familia, bali pia kwa Jeshi la Magereza na jamii kwa ujumla, iliyopoteza mmoja wa viongozi wake waliotumikia kwa uadilifu na kujituma.
Umba alifariki April 16,2026 jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kamanga.
Mwisho.








0 Comments