WILAYA ZA KIMKAKATI ZANUFAIKA NA MATREKTA YA KUPULIZIA.

 


Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.


SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imenunua mitambo au Mashine 16 kwa ajili ya kurahisisha shughuli za upuliziaji na udhibiti wa wadudu wanaoshambulia na kufyonza zao Pamba nchini.


Mitambo hiyo imesambazwa katika wilaya tano za kimkakati katika uzalishaji wa Pamba ambazo ni Meatu, Maswa, Bariadi (Simiyu), Kishapu (Shinyanga) na Igunga (Tabora) na kwamba  zinandelea kufanyiwa majaribio kwa wakulima wenye mashamba makubwa ili kurahisishia upuliziaji.


Akizungumzia mashine hizo, Afisa Uhamasishaji na Maendeleo ya Pamba kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Edward Nyawile, amesema serikalini imenunua na kugawa mashine hizo kwenye wilaya za kimkakati kwa uzalishaji wa Pamba na kwamba zimelenga kuhudumia wakulima wenye mashamba makubwa.



Amesema kuwa mashine hizo zinahuudumia wakulima wa Pamba waliopanda kwa kuzingatia kanuni za kilimo hicho ikiwemo kupanda kwa mistari kwani mtambo huo huendesha na kupitia ukipulizia dawa shambani.


"Mashine hizo zimenunuliwa rasmi katika wilaya za kimkakati za Meatu, Maswa, Bariadi (Simiyu), Igunga (Tabora) na Kishapu (Shinyanga)...lengo ni kuhamasisha Kilimo chenye tija pia kurahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima wetu" amesema.



Awali wakizungumza na waandishi wa Habari za Pamba, wakulima kutoka Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, waliipongeza serikali kwa kuleta Teknolojia za kisasa ambazo zitawarahisishia wakulima shughuli za kilimo ambapo awali walikuwa wanatumia muda mrefu shambani.



Marco Kayanhale, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mwamlapa, alisema awali alikuwa analipa vibarua kupulizia shamba lake, lakini kutokana na ujio wa mashine hizo sasa.atapunguza gharama na muda wa kushinda mashambani.


Marco Kayanhale, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mwamlapa wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu akizungumza na waandishi wa Habari juu ya 

"Miaka ya nyuma tulikuwa tunapulizia kwa solo la mgongoni, sasa tunaomba Serikali imetuletea mashine (Trekta) ya kupulizia... tumeona hapa mashine imerahisisha kazi, katika shamba hili nilikuwa natumia siku nne kupulizia na kuchoka sana, sasa hivi naona unafuu kwenye mashine hii" alisema.


Marco Kubagwa, Mkulima wa kijiji cha Nyanguge wilayani Bariadi, alisema mashine hizo zinarahisisha upuliziaji kwa wakulima wenye mashamba makubwa badala ya kutumia pampu ya mgongoni ambayo ilisababisha uchovu na maumivu, pia mashine hizo zinapulizia mashamba makubwa kwa muda mfupi.


Afisa Kilimo kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), Kijiji cha Mwamlapa, Chongela Selemani, alisema mashine hizo zimerahisisha kazi kwani awali wakulima walitumia siku 2 au 3 kumaliza kupulizia shamba la ekari moja. 


Alisema kuwa wanaendelea na Mafunzo ya umwagiliaji, lakini changamoto wanayokumbana nayo bado wakulima wengi hawazingatii kanuni za kilimo bora ikiwemo kupanda Kwa mistari, lakini wanaendelea kuwabadilisha kupitia mashamba darasa ili wapande kitaalamu.



Mwisho.





Post a Comment

0 Comments